Baba
Mtakatifu Francisco, kama kawaida ya mapema siku ya Jumatano alitoa
katekesi yake kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamekusanyika Vatican.
Mafundisho yake, yalizama katika kuelezea nini maana ya kukiri
“ninasadiki katika Kanisa Moja na Takatifu “.
Papa alianza,
.....Ndugu zangu wapendwa, tunakiri katika sala ya Kanisa, Ninasadiki
katika Kanisa moja na Takatifu, kwa sababu asili yake ni katika Utatu
Mtakatifu wa Mungu, fumbo la umoja na ushirika kamili. Ni Takatifu kwa
sababu limejengwa juu ya Yesu Kristo, na kuhuishwa na Roho wake
Mtakatifu, na kujazwa juu yake na upendo wake na wokovu wake. Lakini
wakati huohuo ndani mwake mna wadhambi ambao kila siku huanguka katika
udhaifu wa dhambi.
Kwa hiyo imani hii tunayokiri, kama waamini
wa Kanisa Moja Takatifu , inatusukuma katika kuwa waongofu na ujasiri
wa kuishi kila siku katika umoja na utakatifu unaotoka kwa Mungu
mwenyewe. Na Yesu Kristo ndiye msingi wetu wa umoja na utakatifu, na
hivyo kama sisi kama hatuko katika umoja na kama hatuko watakatifu, basi
hatuna imani kwake. Lakini pamoja na udhaifu huo bado hajatuacha peke
yetu.
Papa alieleza kuitenga hotuba yake katika vipengere
vitatu, akianza na faraja itokayo kwa Mungu kwamba, waamini hupata
faraja kutoka kwa Yesu, kwa kuwa tangu mwanzo wa kulijenga kanisa lake
aliomba kwa Baba yake, Baba wote wawe na umoja kama wewe Baba ulivyo
ndani yangu nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu ,ili ulimwengu
upate kusadiki kwamba wewe ndiwe uliyenituma(Yn17; 11.21-23) Papa
alieleza na kuongeza kwa njisi gani ilivyo vyema kufahamu kwamba Bwana
alitupenda hadi kuyatoa maisha yake kwa ajili ya sisi wenye dhambi, ili
tupate mastahili ya kuwa katika umoja huu Mtakatifu. Maneno hayo ya
Yesu yanatupa utambuzi kwamba kupitia kwa Yesu pia sisi tunaweza
kuingia katika umoja kamili na upendo wake, na katika roho wake ,
jumuiya za Kristo zinapata dhamana hii kutambuliwa kama jumuiya ya
Kikristo zilizo jengwa katika utakatifu.
Papa aliomba umoja wa
wafuasi wa Yesu, uliosimikwa zaidi ya yote katika sala ya majitoleo
ya mateso na kifo chake msalabani. Kwa ajili hiyo , Papa alitoa mwaliko
kwa watu wote kuendelea kutafakari maneno hayo yaliyo andikwa katika
Injili ya Yohana 11:21-23 akilitaja kuwa ni neno la ujasiri lililotoka
kwa Mungu linalo tuita kila siku katika wogofu. Kupitia kwa Yesu
Kristo, ambaye husali kwa ajili yetu na hasa kwa mateso yake,sis
wabatizwa kama kanisa lake sote tuungane katika umoja nae na Baba na
kati yetu.
Baba Mtakatifu aliendelea kueleza kwa masikitiko
kwamba, kwa bahati mbaya , pamoja na kutambua vyema , dhambi ni kinyume
cha umoja, wivu na chuki na ubinafsi kuwa kinyume cha usharika, bado
tunakaribisha ndani ya roho zetu na katika jumuiya zetu na parokia zetu
dhambi hizi badala ya kukumbatia Mapenzi ya Mungu, yanayo tutaka tukuze
moyo wa kupendana , kukaribishana na kumpenda kila mtu kama Yesu
anavyotupenda sote. Huo ndio utakatifu wa Kanisa , kutambua sura ya
Mungu katika mwingine . Hivyo,tunapokiri imani hii katika sala ya
Nasadiki, tunahimizwa kujali uongofu wetu , kwa kuwa na ujasiri wa
kuishi katika umoja na utakatifu kila siku, kwa utambuzi kwamba unatoka
kwa Mungu. Na kwamba, Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyemwilishwa na kuja
kukaa kati yetu ni chanzo cha umoja wetu na utakatifu, na kama sisi si
wamoja , kama sisi si watu wa Mungu, ni kwa sababu sisi si wafuasi
wake. Hata hivyo, Yesu hatutelekezi, bado yu kado akisubiri tumkaribishe
tena mioyoni mwetu. Kamwe hawi mbali na kanisa lake.
Na Yesu
alitolea sala yake kutoka moyoni kwa Baba yake , akiomba umoja, sisi
tunaweza pia sisi kuwa na umoja kati yetu. Na hivyo kwa maneno hayo,
Yesu alitenda kama wakili wetu kwa Baba, ili sisi pia tuweze kuingia
katika ushirika kamili wa upendo pamoja naye; wakati huo huo, anatoa
dhamana kwetu ya kuwa mashahidi wake wa kiroho, na kwa ajili ya utoaji
wa majibu mazuri zaidi kwa mtu yeyote ambaye anaye uliza habari ya
wokovu na matumaini yetu (cf. 1 Pt 3 , 15).
Papa aliendelea na
kipengere cha pili akirejea Injili ya Yohane 17:21: wote wawe kitu
kimoja, kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yenu, inaweza
wao pia wawe ndani yetu ili ulimwengu upate kuamini kwamba wewe
ulinituma. Papa alifafanua Kanisa tangu mwanzo ndivyo lilivyojengwa
katika umoja kama yalivyokuwa mapenzi ya Yesu. Na kwamba, Matendo ya
Mitume hukumbusha kwamba Wakristo wa kwanza walijulikana kweli kuwa na
"moyo huo wa umoja na roho moja" (Matendo 4 , 32); kisha Mtume Paulo
aliwahimiza wasishau kuwa "mwili mmoja" (1 Kor 12:13).
Lakini
uzoefu wa maisha unatuonyesha kwamba, kuna dhambi nyingi dhidi ya
umoja. Na si tu kufikiri juu ya uzushi mkubwa na ukana Mungu, lakini
pia tunapaswa kufikiria juu ya mapungufu madogomadogo ambayo tunaweza
kuyaita ya kawaida yanayotokea katika jumuiya zetu na hata parokia zetu
ambamo washarika wake wameigiwa na dhambi na kusababisha migawanyiko na
utengano, inayoletea na dhambi ya wivu, chuki, fitina n.k. Papa anasema,
sawa kibindamu tunaona kama ni kawaida lakini si Kikristo! Hii
hutokea hasa wakati tukiuweka ubinafsi katika matarajio na ufanikishaji
wa malengo ya pamoja. Wengi wetu tunawahukumu wengine vibaya kwa
sababu mimi ninataka kufanikisha lililo ndani mwangu kwa kumwangusha
mwingine kwa nia mbaya. Wengi tunaangalia makosa ya wengine zaidi yetu
tukiyafumbia macho badala ya kutazama ujuzi wao. Mtu anajenga moyo wa
kujiona bora zaidi na hivyo kujitenga na mengine na huo ndiyo mwanzo wa
migawanyiko inayotokea hata ndani ya jumuiya za kanisa, ambazo zinapaswa
kuwa mahali pa kuwaungunisha watu na kuw ana roho moja miongoni wao.
Papa
alimalizia na kipengere cha tatu ambamo amezungumzia umuhimu wa
kuchunguza dhamiri akisema kwamba, katika jumuiya ya Kikristo, utengano
ni moja ya dhambi kubwa zaidi, kwa sababu jumuiya ya Kikristo inapaswa
kuwa ishara ya kazi ya Mungu,na si kazi ya shetani. Utengano huharibu
mahusiano, na ni mwanzo wa uharibifu kwa jumuiya na chukizo kwa Mungu.
Kumbe Jumuiya au parokia vinapaswa kuwa mahali pa kukua uwezo wa
kusalimiana yetu, kusamehe na kupendana, kwa kuangalia zaidi na zaidi,
ni mahali pa ushirika na upendo. Na hiyo ndiyo maana ya kusali: Nasadiki
katika Kanisa Moja na Takatifu. Hii ni kulitambua Kanisa kuwa mfano wa
Mungu, lililojazwa huruma yake na neema yake.
Papa alikamilisha
mafundisho haya kwa kutoa mwaliko kwa waamini wote , kufanya tafakari
ndani ya mioyo yao maneno ya Yesu: "Heri wenye kuleta amani, maana
wataitwa wana wa Mungu" (Mt 5,9). Kwa moyo wa dhati, ni kuomba msamaha
kwa nyakati zote tunapokuwa na matukio ya kuleta mgawanyiko au
kutokuelewana ndani ya jamii zetu, licha ya kuwa na ufahamu kwamba,
mgawanyiko huvunja umoja na ushirika katika jumuiya na wala hatuwezi
kuendelea kutembea katika njia ya uongofu ulio imara.Na hivyo tumwombe
Mungu, ili kwamba mahusiano yetu ya kila siku yaweze kuwa zaidi mazuri
na furaha na yenye kutoa mwangwi mzuri katika uhusiano kati yetu na kati
yetu a Yesu na katu yetu na Mungu Baba.