Pia tatizo hilo linachangiwa na mila potofu pamoja na tamaduni, kwa baadhi ya makabila hapa nchini.
Watoto waliopo maeneo ya vijijini ndiyo wanakumbana na mateso ya kuozeshwa ndoa za utotoni kutokana na hali duni ya mfumo mzima wa maisha ya familia zao, na hivyo kushindwa kuendelea na masomo.
Wengi wa watoto hawa hawawezi kupinga suala hilo linapotokea na kwa kuwa ni vijijini inakuwa vigumu kupata msaada wowote wa kisheria.
Pia wapo walimu wakuu shule za msingi na sekondari ni chanzo cha tazito hilo kwa kuwa baadhi yao hushirikiana na wazazi kuwakatiza masomo watoto hao kwa ajili ya kuolewa.
Niliumia sana nilipokutana na mtoto wa miaka 15, aliyeolewa na akiwa na umri wa miaka 12 wakati huo akiwa mwanafunzi wa darasa la nne, katika shule ya msingi Izava iliyopo Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Taarifa hizo nilizipata kutoka kwa majirani wa kijiji nilichokuwepo. Ilikuwa vigumu kuamini tuko hilo, hivyo nililazimika kumtemblea mtoto huyo nyumbani kwake.
Nilihuzunika nilipomkuta mtoto huyo akiwa nyumabani kwake huku kukiwa giza akihangaika kuwasha moto wa kuni. Pembeni yake kulikuwa na mtoto wa mume wake waliopishana mwaka mmoja.
Mtoto huyo alinieleza kwa masikitiko huku machozi yakimtoka, jinsi alivyoachishwa shule na wazazi wake wakishirikiana na mwalimu mkuu wa shule aliyokuwa akisoma.
Bado nasikitika kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo jinsi alivyoweza kumpa mbinu muoaji, ili kuifumbaza jamii iliyowazunguka ama wanafunzi wenzake wasijue kinachoendelea kwa mtoto huyo.
Hata hivyo, mtoto huyo anasema mwaka huu angekuwa kidato cha kwanza kama angeweza kumaliza elimu yake ya msingi.
Najua kwamba mwalimu ni mlezi wa mwanafunzi wakishirikaana na wazazi, lakini kwa hili imekuwa ni tofauti kabisa.
Ni watoto wangapi hapa nchini waliofanyiwa ukatili wa kuozeshwa ndoa za utotoni hasa waliopembezoni mwa mijni?
Hali duni ya maisha yetu isiwe sababu ya kuwadhulumu watoto wetu kupata haki zao za msingi.
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimekuwa mstari wa mbele kupigania haki za wanawake na watoto, hivyo ni vema Tamwa wakaweka kambi vijijini, ili kubaini hali halisi ilivyopo huko ambapo watoto wengi huachishwa shule na kuolewa.
Niwasihi wazazi tusiwafanye watoto wao mradi wa kujipatia kipato na kuwaharibia mfumo bora wa maisha yao.
Pia tatizo hili ni letu sote wanajamii, hivyo kinachofanywa na Tamwa kinapaswa kiungwe mkono, ili kukabiliana na hali hiyo na kuweza kuondoa unyanyasaji kwa watoto waliochini ya umri wa miaka 18 nchini.
Mtoto wa kike ni mkombozi kwa jamii hasa akipata elimu, hivyo anahitaji kukombolewa, ili kuondokana na ukatili huo.
Watoto wanaolewa mapema hawapati elimu na nafasi ya kujipanua kiakili, hivyo hukosa fursa ya kujikuza kiuchumi hali inayosababisha kukosa uwezo wa kuzikomboa familia zao kutokana na umasikini uliopo.
Tunapaswa kubadili mtazamo wa familia na jamii kwa ujumla kuwa mtoto wa kike ana maamuzi yake na matarajio ya baadae hivyo, tusipoteze ndoto za watoto wetu.