
Stars kesho watawakabili Msumbiji katika mechi ya kwanza ya hatua ya mwisho ya kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi kupigania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika zitakazopigwa mwakani nchini Morocco.
Samatta, amesema kwa ari ya wachezaji wa timu hiyo, wana uhakika wa kuibuka na ushindi katika mechi hiyo, hasa wakizingatia kuwa wao watakuwa wakicheza mbele ya wapenzi na mashabiki.
Alisema hayo jana wakati akielezea maandalizi ya timu hiyo na matumaini yao kuelekea mechi hiyo ambayo ni muhimu kwa Stars kushinda kabla ya wiki mbili zijazo kusafiri hadi Maputo, Msumbiji kwa mechi ya marudiano.
“Watu wasiwe na hofu na mechi yetu dhidi ya Msumbiji, naamini kila mchezaji yupo fiti kupigania ushindi, kitu muhimu ni wapenzi na mashabiki kujitokeza kwa wingi kutushangalia,” alisema Samatta.
Naye Thomas Ulimwengu, alisema licha ya wao kuchelewa kuungana na wenzao, lakini wapo fiti kama ilivyo wachezaji wengine, hivyo haoni sababu ya kufungwa na Msumbiji.
Mbali ya nyota hao wa kimataifa, Nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Canavaro’, alisema licha ya baadhi ya wachezaji kuwa katika mfungo, anajua haitaharibu kitu kwa kuwa kila mmoja wao ana imani yake.
“Sisi kusema kweli tuko vizuri na kuhusu swaumu, hakuna shida kabisa, hiyo ni imani ya mchezaji mwenyewe, ila Watanzania mje kwa wingi tuko vizuri,” alisema Canavaro.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, viingilio katika mechi hiyo ni sh. 7,000 na sh. 30,000 kwa viti maalum, huku tiketi (za kielektroniki) zikiuzwa pia katika magari kwenye vituo mbalimbali.
Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Buguruni Shell, Dar Live Mbagala, Ferry Magogoni, Kigamboni, OilCom Chang’ombe, OilCom Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa (Kariakoo), TCC Club Chang’ombe na Uwanja wa Taifa.
“Tiketi zinapatikana kupitia M-Pesa kwa kupiga *150*00# kisha bonyeza 4, bonyeza tena 4 kisha weka namba ya kampuni 173399 kisha ingiza 7000 kama namba ya kumbukumbu ya malipo,” alisema Wambura.
Alisema baada ya hapo andika tena 7000 weka kiasi, kisha weka namba ya siri na baadaye bonyeza 1 kukubali.
Wambura alisema baada ya hapo, mhusika atapokea ujumbe wenye orodha ya vituo vya MaxMalipo vya kuchukua tiketi akiwa na namba ya uhakiki wa malipo yake.
Wambura alisema, vituo vya MaxMalipo vya kuchukulia tiketi ni mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Samora/Ohio, maduka makubwa ya Uchumi Supermarket (Quality Centre) na Tabata Segerea.
Maeneo mengine ni Kituo cha Dadadala Makumbusho, Sheer Illussions (Millennium Tower na Mlimani City), maduka makubwa ya TSN Supermarket (City Centre, Kibo Tegeta na Upanga).
Mengine ni Vodashop (Ubungo na Mill Pamba), Shop Mwenge (Born to Shine), Puma Petrol Station (Mwenge na Uwanja wa Ndege), Engen Petrol Station (Mbezi Beach), Big Bon Petrol Station (Kariakoo, Sinza Mori, Mbagala na Temeke), YMCA (Posta Mpya), City Sports Lounge (Posta), Uwanja wa Taifa) na Uwanja wa Karume.